Maliza Vizuri!

Maliza Vizuri!

AI
Neno la Leo by Neno la Leo 255
S3 · E61
Sep 30, 2026
24:16

Episode notes

🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

Leo kupitia 1 Samweli 30:23–26 na 31:1–4 tunafunga mwezi wetu na wakati huohuo tunafika mwisho wa safari yetu kupitia kitabu cha 1 Samweli.

Na Biblia inatuacha na picha mbili tofauti sana:

Daudi na Sauli.

Daudi anatoka katika kipindi kigumu sana kule Ziklagi. Ameona mji wake ukiteketea. Amelia mpaka hana nguvu. Watu wake wametaka kumpiga mawe.

Lakini Daudi akajitia nguvu katika Bwana, akamwuliza Mungu hatua inayofuata na mwisho akapata ushindi.

Baada ya ushindi, baadhi ya watu wake wanataka kujichukulia nyara na kuwanyima wale waliokuwa wamechoka na kubaki nyuma.

Lakini Daudi anasema kwa maana:

“Msifanye hivyo na kile Bwana alichotupa.”

Hapo tunaona kitu kuhusu moyo wa Daudi.

Baada ya ushindi hakusema, “Angalieni nilichofanya.”

Alikumbuka:

“Bwana ndiye aliyetupa.”

Na hata kile alichopokea hakukishikilia kwa ajili yake mwenyewe. Akagawa na wengine.

Lakini tunapofungua sura ya mwisho ya 1 Samweli, tunakutana na picha nyingine.

Sauli anafika mwisho wa safari yake.

Na mwisho wake ni wa kusikitisha sana kwa sababu Sauli alianza vizuri.

Alichaguliwa. Akapakwa mafuta. Roho wa Mungu akaja juu yake. Akapewa nafasi kubwa ya kuliongoza taifa.

Lakini hatua kwa hatua moyo wake ukaanza kubadilika.

Kutokutii. Hofu ya watu. Wivu. Hasira. Kulinda nafasi yake.

Mpaka Daudi, mtu ambaye angeweza kuwa msaada kwake, akawa mtu ambaye Sauli alitumia miaka mingi akimfukuza.

Halafu tunamtazama Daudi.

Na hapa tunahitaji kukumbuka:

Daudi hakuwa perfect.

Tumemwona akiogopa.

Tumemwona akichoka.

Tumemwona akiwa karibu kulipiza kisasi.

Tumemwona akifanya maamuzi akiwa chini ya pressure.

Tumemwona akilia mpaka hana nguvu tena za kulia.

Kwa hiyo tofauti kati ya Daudi na Sauli haikuwa kwamba mmoja hakuwahi kukosea.

Tofauti muhimu tunayokutana nayo tena na tena ni hii:

Daudi aliendelea kurudi kwa Mungu.

Akichanganyikiwa, anamwuliza Mungu.

Akidhoofika, anajitia nguvu katika Bwana.

Akisahihishwa na Abigaili, anakubali kusahihishwa.

Akipata ushindi, anakumbuka aliyempa ushindi.

“Bwana ndiye aliyetupa.”

Na hapo tunarudi kwenye somo tuliloanza nalo mwezi huu:

Mungu anaangalia moyo.

Unaweza kuwa na karama.

Unaweza kuwa na nafasi.

Unaweza kuwa na calling.

Unaweza kuanza vizuri sana.

Lakini swali muhimu zaidi ni:

Moyo wako unaendelea kwenda upande gani?

Paulo alipofika karibu na mwisho wa safari yake hakusema tu, “Nilianza vizuri.”

Alisema:

“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda.”

Mwendo nimeumaliza.

Na tunapofunga mwezi, labda hilo ndilo swali tunalopaswa kubaki nalo:

Baada ya yote niliyopitia mwezi huu, moyo wangu uko wapi?

Je, bado ninamtafuta Mungu?

Je, nimekuwa karibu naye zaidi au nimeanza kwenda mbali?

Kuna hasira ninayobeba?

Kuna wivu?

Kuna kutokusamehe?

Kuna jambo Mungu amekuwa akiniambia niliachilie lakini bado nimelishikilia?

Kuna sehemu ninahitaji kurudi kwake?

Kwa sababu safari ya Sauli na Daudi inatuachia ukumbusho mzito:

Sio tu jinsi unavyoanza. Ni jinsi unavyomaliza.

Na kwa neema ya Mungu, tusitafute tu kuanza vizuri.

Tuombe tumalize vizuri. 🙏📖

Karibu tusikilize, tutafakari na tufunge mwezi pamoja katika Neno la Leo.