

Usilishe Tamaa Isiyofaa Moyoni
Note sull'episodio
🎙️ Leo kwenye Neno la Leo
Leo kupitia 2 Samweli 13:1–2 tunaingia katika sehemu ngumu na yenye huzuni katika familia ya Daudi.
Tunamkuta Amnoni akianza kuwa na tamaa isiyofaa kwa Tamari, dada yake wa kambo.
Lakini kuna jambo muhimu ambalo maandiko yanatuonyesha kabla hata hatujafika kwenye kile kitakachotokea baadaye.
Amnoni anaendelea kuibeba na kuilisha tamaa hiyo moyoni mpaka inamtesa.
Na hapa tunahitaji kutofautisha mambo mawili.
Wazo linalopita kichwani na uamuzi wa kulipa nafasi ni vitu viwili tofauti.
Hatuchagui kila wazo linalotokea akilini. Hatuchagui kila temptation inayojitokeza.
Lakini tuna responsibility juu ya kile tunachokiruhusu kikae, kikue na kuanza kutawala mawazo yetu.
Yakobo 1:14–15 anatupa picha ya jinsi tamaa inavyoweza kukua mpaka kuzaa dhambi.
Na hapo ndipo simulizi la Amnoni linakuwa onyo kubwa kwetu.
Tatizo lake halikuanza siku alipomdhuru Tamari.
Lilikuwa limeanza moyoni.
Kabla ya tendo kulikuwa na tamaa.
Kabla ya mpango kulikuwa na mawazo yaliyokuwa yakipewa nafasi.
Na kabla wengine hawajaona tatizo, tayari kulikuwa na vita ambavyo Amnoni alikuwa akivipoteza ndani yake.
Hilo linatuuliza swali muhimu:
Ni kitu gani ninachokilisha moyoni ambacho najua hakipaswi kukua?
Huenda si tamaa ya kingono.
Inaweza kuwa wivu.
Hasira.
Kisasi.
Tamaa ya mali.
Kiburi.
Kutamani maisha ya mtu mwingine.
Au fantasy ambayo tunajua inatupeleka mahali pasipo sahihi.
Mara nyingi tunataka kupambana na dhambi ikiwa tayari imekuwa kubwa. Lakini hekima ni kuikabili ikiwa bado ni mbegu.
Usisubiri wazo baya ligeuke kuwa tendo ndipo uanze kupigana nalo.
Na hapa kuna distinction muhimu pia.
Kujaribiwa hakukufanyi moja kwa moja kuwa mtu mbaya. Wazo baya kujitokeza akilini halimaanishi tayari umelitenda.
Swali ni:
Utafanya nini nalo?
Utalikataa au utalirudia tena na tena?
Utalileta mbele za Mungu au utalificha na kulikuza?
Utalikata mapema au utasubiri mpaka likuanze kukutawala?
Wafilipi 4:8 inatukumbusha kuelekeza mawazo yetu katika yaliyo ya kweli, yenye heshima na yaliyo safi.
Kwa sababu kile tunachoruhusu kikae akilini kinaweza kuanza kutengeneza kile tunachotamani. Na kile tunachotamani kinaweza kuanza kuongoza kile tunachofanya.
Kwa hiyo usidharau vita vinavyoendelea moyoni.
Kuna vita ambavyo ni rahisi zaidi kuvishinda vikiwa bado ni mawazo kuliko baada ya kuwa matendo.
Usilishe kile ambacho hutaki kikuze ndani yako.
Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨