

Unaweza Kulia na Bado Ukawa na Imani!
Note sull'episodio
🎙️ Leo kwenye Neno la Leo
Leo kupitia 1 Samweli 30:3–6 tunakutana na moja ya siku nzito zaidi katika maisha ya Daudi.
Daudi na watu wake wanarudi Ziklagi wakitarajia kurudi nyumbani. Lakini wanapofika, wanakuta mji umechomwa moto na familia zao zimechukuliwa mateka.
Biblia inasema:
“Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakapaza sauti zao wakalia hata walipokuwa hawana nguvu tena za kulia.”
Hawa ni mashujaa.
Wamepitia vita. Wameishi jangwani. Wamekabiliana na hatari nyingi.
Lakini leo wanalia.
Na Daudi analia pamoja nao.
Huyu ni Daudi aliyesimama mbele ya Goliathi. Huyu ni Daudi aliyepakwa mafuta kuwa mfalme. Huyu ni Daudi ambaye tumemfuatilia tukiona imani na ujasiri wake.
Lakini leo hana motivational speech.
Ana machozi.
Na hapo tunajifunza jambo muhimu: imani haimaanishi kwamba hutawahi kuvunjika moyo.
Kuna maumivu ambayo huwezi kuyafunika kwa maneno mazuri. Kuna siku ambazo jambo la kiroho zaidi unaloweza kufanya ni kuacha kujifanya uko sawa na kumwambia Mungu:
“Bwana, hili limeniumiza.”
Lakini simulizi la Daudi halimaliziki kwenye machozi.
Baada ya kulia mpaka hana nguvu tena, hali inakuwa mbaya zaidi. Watu wake wenyewe wanamgeukia. Wakiwa katika uchungu wanaanza hata kuzungumza kuhusu kumpiga mawe.
Fikiria Daudi hapo.
Nyumbani hakuna. Familia haipo. Watu aliowaongoza wanamlaumu.
Yonathani hayupo.
Samueli hayupo.
Hakuna mtu wa kumshika mkono na kumwambia, “Daudi, endelea.”
Ndipo Biblia inasema:
“Lakini Daudi akajitia nguvu katika Bwana Mungu wake.”
Hapo ndipo moyo wa episode yetu ulipo.
Kuna nyakati Mungu atatumia Yonathani kukutia nguvu. Tuliona hilo katika 1 Samweli 23:16.
Lakini kuna siku Yonathani hatakuwepo.
Na katika siku hizo, tunahitaji kujifunza kwenda kwa Mungu wenyewe.
Si kujifanya hatuumii. Si kukataa machozi. Bali kusema:
“Bwana, nimeumia. Nimechoka. Sina nguvu tena. Lakini bado wewe ni Mungu wangu. Nitie nguvu.”
Hii ndiyo imani inayokomaa.
Imani ambayo inaweza kulia mbele za Mungu na bado kumshikilia Mungu.
Kwa hiyo kama unapitia siku nzito, usijione kwamba umepoteza imani kwa sababu umelia.
Lia ikiwa unaumia.
Mweleze Mungu ukweli wa moyo wako.
Lakini usiishie kwenye machozi.
Rudi kwa Mungu ambaye anaweza kukupa nguvu ya kusimama tena.
Kwa sababu unaweza kulia na bado ukawa na imani.
Machozi si mwisho wa hadithi.
Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨