

Usijilipizie Kisasi Hata Ukipewa Nafasi
Note sull'episodio
🎙️ Leo kwenye Neno la Leo
Leo kupitia 1 Samweli 26:9–11 tunamwona Daudi akikabiliwa tena na mtihani ambao tayari aliwahi kuupita.
Mara ya kwanza Sauli aliingia katika pango ambamo Daudi alikuwa amejificha. Daudi alikuwa na nafasi ya kumuua lakini akakataa.
Sasa inatokea tena.
Daudi na Abishai wanaingia kambini usiku na kumkuta Sauli amelala. Mkuki wake uko karibu na kichwa chake. Abishai anaangalia mazingira na anafikia conclusion ambayo wengi wetu tungeweza kufikia: “Mungu amemtia adui yako mikononi mwako.”
Fikiria kama ungekuwa Daudi. Mara ya kwanza pangoni. Sasa mara ya pili kambini.
Angeweza kusema, “Mara mbili sasa? Surely hii ni confirmation kutoka kwa Mungu!”
Lakini Daudi anakataa.
Kwa sababu kurudiwa kwa nafasi hakubadilishi jambo lisilo sahihi kuwa sahihi.
Na hilo ni somo muhimu sana kwetu. Wakati mwingine mlango unafunguka mara moja na tunajiuliza kama ni Mungu. Halafu jambo lilelile linatokea tena na tunasema, “Sasa nimepata confirmation!”
Lakini si lazima.
Confirmation ya kweli haiwezi kutufanya tupuuze kile ambacho tayari tunajua ni sahihi mbele za Mungu. Nafasi bado inahitaji kupimwa kwa Neno, hekima na tabia ya Mungu.
Na kuna jambo jingine zuri sana katika moyo wa Daudi. Anaamini kwamba kama kweli Mungu amemchagua kuwa mfalme, hahitajiki kumuua Sauli ili kusaidia ahadi ya Mungu itimie.
Hilo ni Neno kubwa kwetu.
Huhitaji kufanya jambo baya ili kusaidia mpango mzuri wa Mungu utimie.
Huhitaji kudanganya ili kupata kile Mungu amekuandalia. Huhitaji kumwangusha mwingine ili wewe upande. Huhitaji kulipiza kisasi ili Mungu akutetee. Huhitaji kutumia njia isiyo sahihi kwa sababu tu mwisho unaonekana mzuri.
Mungu hahitaji dhambi yako ili kutimiza kusudi lake.
Kama jambo limetoka kwake, unaweza kusubiri wakati wake na kulipokea kwa njia inayomheshimu.
Kwa hiyo usiangalie tu mara ngapi mlango umefunguka.
Uliza pia:
“Nikiingia katika mlango huu, nitakuwa namheshimu Mungu?”
Kwa sababu nafasi ikija mara mbili, si lazima iwe confirmation ya Mungu.
Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨