

Waisraeli Walipotamani Kile Wasichokihitaji!
Note sull'episodio
🎙️ Leo kwenye Neno la Leo
Leo kupitia 1 Samweli 8:6–7 tunafika katika hatua muhimu katika historia ya Israeli. Waisraeli wanamtaka mfalme ili wawe “kama mataifa mengine.” Samweli anahuzunika lakini Mungu anamfunulia tatizo kubwa zaidi: “Si wewe waliyekukataa bali wamenikataa mimi nisiwe mfalme wao.” Walikuwa na Mungu akiwaongoza lakini wakaanza kutamani mfumo waliouona kwa wengine. Neno la leo linatufanya tujiulize kama nasi wakati mwingine tunatamani vitu si kwa sababu tunavihitaji au ni mapenzi ya Mungu bali kwa sababu tunaona wengine wanavyo. Tunaweza kutamani kazi, fedha, mahusiano, nafasi au maisha ya mtu mwingine mpaka tukashindwa kuona kile ambacho Mungu tayari ametupa. Si kila tunachotamani ndicho tunachohitaji na si kila kitu kizuri kwa mwingine ni kizuri kwa kusudi la Mungu juu yetu. Je, tunaweza kumwamini Mungu hata pale mapenzi yake yanapotofautiana na yale tunayotamani? Wakati mwingine baraka si Mungu kutupa tunachotaka bali kutuzuia tusipate kile ambacho tunadhani tunahitaji.
Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨