

Usifanye Maamuzi Makubwa Ukiwa Umechoka na Kuogopa!
Notas del episodio
🎙️ Leo kwenye Neno la Leo
Leo kupitia 1 Samweli 27:1 tunakutana na Daudi katika hali ambayo huenda wengi wetu tunaifahamu.
Jana alikuwa amesimama imara katika imani. Alikuwa na nafasi nyingine ya kumuua Sauli lakini akakataa. Alikuwa tayari kumwachia Mungu matokeo.
Lakini leo tunamsikia Daudi akisema moyoni mwake:
“Siku moja nitaangamia kwa mkono wa Sauli.”
Ngoja kidogo.
Huyu si Daudi aliyemshinda Goliathi? Si huyu ambaye Mungu amemwokoa kutoka kwa Sauli tena na tena? Si huyu ambaye tayari amepakwa mafuta kwa ajili ya kusudi kubwa?
Ndiyo.
Lakini Daudi amechoka.
Amekimbia kwa muda mrefu. Leo yuko pangoni, kesho jangwani na kesho kutwa sehemu nyingine. Ameishi muda mrefu chini ya pressure ya kujiuliza Sauli atampata lini.
Na sasa uchovu unaanza kuzungumza kuhusu kesho yake.
Hapo ndipo tunapata somo muhimu sana. Wakati mwingine tunapokuwa tumechoka, hofu huanza kutafsiri maisha yetu. Tunaanza kuona kama haiwezekani kile ambacho jana tuliamini kinawezekana.
Baada ya kuomba muda mrefu tunasema, “Labda Mungu hatajibu.” Baada ya kusubiri tunasema, “Labda haitabadilika.” Baada ya kupambana kwa muda mrefu tunasema, “Labda niache tu.”
Lakini hisia ya leo si lazima iwe ukweli kuhusu kesho.
Kumbuka historia ya Daudi. Sauli alikuwa amemtafuta mara nyingi lakini Mungu alikuwa amemhifadhi. Kilichobadilika katika mstari huu si uaminifu wa Mungu. Daudi amechoka.
Na hilo linatufundisha kuwa makini sana na maamuzi makubwa tunapokuwa tumechoka, tumeumia au tunaogopa.
Haimaanishi tusifanye maamuzi magumu. Wakati mwingine mabadiliko yanahitajika. Lakini kabla ya kufanya uamuzi mkubwa, huenda tunahitaji kwanza kupumzika, kuomba, kutafuta ushauri wenye hekima na kupata perspective tena.
Usiache uchovu wa muda mfupi ukushawishi kwamba Mungu amefuta kila alichokuwa akifanya katika maisha yako.
Kabla hujasema, “Imeisha,” kumbuka jinsi Mungu alivyokubeba mpaka hapa.
Kabla hujasema, “Sitaweza,” jiulize kama ni ukweli unaozungumza au uchovu.
Na kabla hujabadilisha kila kitu kwa sababu ya hofu ya leo, rudi mbele za Mungu.
Kwa sababu wakati mwingine unachohitaji si mpango mpya.
Unahitaji nguvu mpya.
Usiruhusu uchovu wa leo uamue kesho yako.
Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨